Na.Mashavu Abdi
Wanawake
wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi nchini wametakiwa kujitokeza kugombea
nafasi za uongozi na kuepuka vikwazo vinavyyowekwa na baadhi ya watu wenye nia
ya kurudisha nyuma ushiriki wa wanawake wa kufikia lengo la usawa wa 50 kwa 50
katika uongozi.
Mkurugenzi
TAMWA-ZNZ Dkt. Mzuri Issa ameyasema hayo katika mkutano na wadau wa masuala ya
wanawake na uongozi kujadili unyanyasaji wa wanawake mitandaoni huko huko ofisi
ya TAMWA-ZNZ Tunguu Wilaya ya kati Unguja.
Dkt.
Mzuri alieleza kuwa, wakati umefika kwa wanawake kujitokeza kugombea nafasi za
uongozi kwa kujiamini na kushinda changamoto hizo kwani wadau mbali mbali
wanachukua jitihada kuhakikisha usawa wa kijinsia katika uongozi unasimamiwa na
kufanya kazi ipasavyo.
‘’Kwa
sasa tumepata fursa nyengine ya kuwanyanyua wanawake na kuwawekea mazingira
mazuri ili waweze kujiona wako salama wanaposhiriki katika nafasi za uongozi na
kufikia usawa wa 50 kwa 50", alieleza Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi
TAMWA-ZNZ.
Akiwasilisha
mada kuhusu rushwa ya ngono katika mkutano huo Afisa elimu Taasisi ya
Kupambambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) Yussuf Juma Suleiman amesema
katiba ya Zanzibar pamoja na mikataba ya kimataifa imetoa nafasi sawa kwa wanawake
na wanaume kushiriki katika uongozi hivyo ni vyema kila mmoja kuchukuwa hatua
kuhakikisha usawa katika nafasi za uongozi unapatikana.
"
Kutungwa kwa sheria za kimataifa pamoja na mikataba mbalimbali ukiwemo mkataba
wa Afrika wa haki za wanawake na watoto na mkataba wa kuondoa aina zote za
ubaguzi dhidi ya wanawake, ni moja wapo ya mifano michache ya kupambana na
unyanyasaji wa kijinsia (rushwa ya ngono)’’ Yussuf Juma Suleiman, Afisa elimu
kutoka ZAECA.
Kwa
upande wake mwakilishi kutoka ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Zanzibar Abdulrazak
S. Ali amesema awali wanawake walipitia changamoto nyingi katika kugombania
nafasi za uongozi zikiwemo uchumi mdogo, mfumo wa uteuzi ndani ya vyama vya
siasa, ubaguzi, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia pamoja na kukosa nafasi
katika vyombo vya maamuzi ambapo kwa sasa changamoto hizo zimepatiwa
ufumbuzi.
“Mwaka
2024 kumefanyika marekebisho makubwa ambayo yatapelekea fursa zaidi kwa
wanawake kuweza kupata nafasi mbali mbali ndani ya vyama vya siasa, maboresho
hayo yamezingatia jinsia na ujumuishi, kuongezwa kwa kifungu cha 10 C ndani ya
marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2024 ambayo yatasaidia uwajibika
kwa vyama vya siasa kuwa na sera ya jinsia kwa muda wote’’ ameeleza Abdulrazak
S. Ali.
Kwa
upande mwengine amewataka wanawake kuweka imani kwa Ofisi ya Msajili wa vyama
vya siasa kwani iko mstari wa mbele kuhakikisha usawa wa jinsia unapatikana
katika vyama vya siasa.
'' Tuwe na imani na Ofisi ya msajili wa vyama
vya siasa kwani tayari imeanzisha dawati la jinsia na kupokea kesi za masuala
yanayohusiana na jinsia bila ya upendeleo na kuzipatia ufumbuzi", amesisitiza
Abdulrazak S. Ali.
Akifunga
mkutano huo Mjumbe wa Bodi TAMWA-ZNZ Hawra Shamte, amewaomba wadau kuelimisha
jamii umuhimu wa wanawake kugombea nafasi za uongozi sambamba kukomesha vitendo
vya unyanyasaji mtandaoni na rushwa ya ngono dhidi ya wanawake.
Mkutano
huo wa siku moja umewashirikisha wadau kutoka taasisi za Serikali na zisizo za
Serikali, waandishi wa habari na wahariri kutoka vyombo mbali mbali vya habari
kujadili masuala ya wanawake na uongozi ikiwemo unyanyasaji wa wanawake
mitandaoni.
MWISHO
No comments:
Post a Comment