Na, Fatma Rajab
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema kufanyika kwa Tamasha la Kilimo hai
ni hatua moja wapo ya kuelekea kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya
Zanzibar 2050, ambayo inalenga kuwa na maisha bora, endelevu na yenye ustahmilivu
kwa Wazanzibari wote.
Ayamesemwa hayo kwa niaba
ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi
katika Tamasha la Kilimo hai la Mwaka 2024 lililofanyika katika Viwanja vya
Maonesho ya Kilimo Nanenane Dole Wilaya ya Magharibi “ A” Unguja.
Amesema kuwa kufanyika kwa
Tamasha hilo hapa Nchini kunapelekea kuwa na Utalii endelevu, kilimo cha asili,
ustahamilivu wa hali ya hewa na kufikia malengo ya Kitaifa na dhamira ya
Ulimwengu kwa Maendeleo endelevu.(SDGs)
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar amesema dhamira ya kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha Utalii endelevu
na kilimo hai imeanza kuzaa matunda ambapo jitihada mbali mbali zinaendelea
kuchukuliwa ili kukuza uchumi na kulinda mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa
na vijavyo.
Aidha Mhe.Hemed amesema kilimo hai ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula, kuimarisha Afya na kulinda mazingira kwa kuiwezesha jamii kupata vyanzo vipya vya maisha pamoja na kuimarisha ustahmilivu wa mifumo ya kilimo dhidi ya mabadiliko ya Tabianchi.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaombele katika mipango inayounga mkono mbinu mpya za kilimo hai, kuanzia kilimo hadi utengenezaji wa bidhaa za kilimo hai zinazoongeza thamani kwenye uchumi wa Zanzibar.
Nae Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo inajipanga kufanya jitihada za hali ya juu kwa kuwashajihisha wakulima na wananchi kwa ujumla kufanya Kilimo hai chenye kupunguza matumizi ya viatilifu sumu, kulinda mazingira na kuimarisha Afya ya Mlaji.
Shamata amesema Wizara
ya Kilimo itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha Tamasha la kilimo hai
linaleta Tija kwa kuongezeka kwa Chakula na kukua kwa uchumi kupitia Sekta ya
Kilimo.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Kilimo hai Tanzania Dkt. Mwatima Abdalla Juma amesema Kilimo hai kinazidi
kukuwa kwa kasi Duniani ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wameweza
kuandaa Mkakati wa Kilimo hai Afrika na kutoa nafasi kwa nchi mbali mbali kuja
kujifunza Tanzani mbinu na mipango ya
kuendeleza Kilimo hai.
Dkt. Mwatima amesema
chamgamoto kubwa katika kuendeleza Kilimo hai Tanzania inatokana na kuendeleza
matumizi ya Viatilifu sumu katika Kilimo ambavyo vinachangia kuongezeka kwa
maradhi mbali mbali nchini, hivyo ameiomba Serikali kusimamia kuondoka kwa
viatilifu sumu ili kuendeleza dhana ya
kilimo hai nchini.
Aidha Dkt. Mwatima ameiomba
serikali kuwapatiwa ruzuku kwa ajili ya kilimo hai ambayo itatumika kwa
kuwasaidia vijana kufanya utafiti utakao ibua mbinu mbali mbali za kuimarisha
kilimo hai sambamba kuiomba Serikali kuridhia Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar(SUZA) kuwa kitovu cha Kilimo hai hapa Zanzibar.
Mapema Mkurugenzi kutoka
Taasisi ya Kilimo hai Zanzibar Ikram Ramadhan soraga amesema lengo la Tamasha
la kilimo hai ni kuweka msingi wa maendeleo endelevu pamoja na kukuza uwelewa
kwa jamii juu ya kukuza mbinu mpya za kilimo hai Zanzibar.
Soraga amesema Tamasha la
Kilimo hai linatoa fursa ya kuwaunganisha pamoja wakulima nchini pamoja na
kuwatafutia soko ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuimarisha kilimo na kukuza
utalii Zanzibar.
Mapema mkamu wa pili wa
rais wa zanzibar ametembelea mabanda ya wajasiriamali,taasisi za serikali na
binafsi pamoja na kujionesha shughuli mbali mbali zinazofanywa na taasisi hizo.
No comments:
Post a Comment