Na, Mwandishi Wetu.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussen Ali Mwinyi amesema
Tanzania imekuwa ikuchukua jitihada
mbali mbali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa sheria za dawa za kulevya hapa nchini
Ameyasema hayo katika
hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.
Hemed Suleiman Abdulla wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Kamisheni ya
Kupambana na dawa za kulevya kwa nchi zilizo Mashariki na Kusini mwa Afrika uliofanyika
katika Ukumbi wa Hotel ya Verde Mtoni
Zanzibar.
Amesema Tanzania
imedhamiria kutekeleza Sera na mikakati madhubuti ya udhibiti wa dawa za
kulevya kwa kudhibiti utengenezaji, uingizwaji, usafirishaji na usambazaji wa
dawa za kulevya nchini ili kupunguza athari zitokanazo na matumizi ya dawa za
kulevya ikiwemo vitendo vya kihalifu, biashara haramu, utakatishaji wa fedha na
ugaidi.
Rais Dkt Mwinyi amesema
kuwa Tanzania imekuwa ikiimarisha ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa katika
kukabiliana na dawa za kulevya kwa kuzijengea uwezo Taasisi zinazoshiriki
katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kuweza kufikia lengo la
kutokomeza matumizi ya madawa hayo hapa nchini.
Aidha Dkt Mwinyi amesema Tanzania inatambua umuhimu wa kuwa na sera madhubuti yenye kutoa miongozo ya kisheria, tiba, elimu yenye kuainisha miongozo jumuishi na ushirikiano kwenye ngazi zote ikiwemo kujikita katika kinga na kutambua mapema viashiria vya biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza
Sambamba na hayo Rais Dkt.
Mwinyi amevipongeza vyombo vya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini
kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kukabiliana na kupambana na dawa za
kulevya kwa lengo la kuhakikisha Tanzania na Watanzania wanakuwa salama
kutokana janga la dawa za kulevya linaloathiri Afya na Ustawi wa Wananchi hasa
vijana.
Nae Waziri wa Mambo ya
Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhandisi HAMAD YUSSUF MASAUNI amesema
Jitihada mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali zote Mbili kwa
kusimamia kikamilifu sheria za kudhibiti dawa za kulevya kwa kudhibiti
usambazaji, Uuzaji na utumiaji wa dawa.
Amesema Serikali kupitia
Mamlaka husika za kupambana na dawa za kulevya zimekuwa zikitoa elimu kwa wananchi na waathirika wa dawa hizo
kupitia vyombo vya habari pamoja na kuwatembelea katika vituo vya vya tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya.
Mhe. MASAUNI amefahamisha
kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vimekuwa vikipambana kikamilifu kuhakikisha
vinadhibiti uingizwaji wa dawa ya kulevya kwa kuimarisha ulinzi hasa katika
maeneo ya mipakani ambayo hutumika kwa kuingizia dawa hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Tume ya Kupambana na dawa za kulevya kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika Mhe. KGALEMA MONTLANTHE amesema dawa za kulevya kwa sasa ni janga hatari
duniani kote hivyo Sera na Mikakati madhubuti inahitajika ili kutokomeza kabisa dawa hizo hasa kwa nchi wanachama.
Amesema Tume ya kupambana
na dawa za kulevya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wanaendelea
kutafuta mbinu mpya na Sera jumuishi za kukabiliana na dawa za kulevya
kwa lengo la kuwadhibiti wauzaji, wasambazaji na watumiaji wa dawa hizo
Amesema Mkutano huo wa siku
mbili utatoa fursa kwa washiriki
kubadilishana Ujuzi na mbinu bali mbali za kufukia lengo la kudhibiti na
kutokomeza dawa za kulevya kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
No comments:
Post a Comment