Na Fatma Rajab.
Wahasibu wanawake Tanzania
wametakiwa kuweka mikakati Imara na thabiti ya kuleta mabadiliko chanya katika
jamii na Taifa kwa ujumla ili kuweza kutanua wigo mpana wa kuhamasisha usawa na
haki kwa wanawake na wasichana Tanzania.
Hayo yamesemwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. HEMED
SULEIMAN ABDULLA wakati akifungua Kongamano la Saba(7) la Uongozi la Wanawake
Wahasibu Tanzania kwa Niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Samia Suluhu Hassan Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya
Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema wahasibu wanawake wana fursa ya kujenga mtandao Imara wa kusaidiana na kuhamasishana kufikia maendeleo waaliokusudia hasa katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Rais Dkt. Samia amesema Serikali
itaendelea kuwa washirika wa kimkakati na kusimama pamoja na TAWCA katika
kuboresha mazingira ya kazi, kuwekeza katika elimu, fursa sawa za maendeleo
pamoja na kuondoa vikwazo dhidi ya
wanawake kwa kuwaandaa kuwa viongozi wa kesho wanaotokana na wanawake wahasibu
nchini.
Aidha Dkt Samia amesema
kuwa TAWCA imekuwa mstari wa Mbele katika kuwainua wajasiriamali kwa kuwapa
taaluma za kifedha na stadi za maisha ili kuweza kuyafikia malengo waliojiwekea
katika biashara zao.
Dkt Samia amekipongeza chama cha wahasibu wanawake Tanzania kwa shuhuli mbali mbali wanazozifanya ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya biashara na ujasiriamali kwa wanawake, kuwasaidia wahasibu wachanga kuweza kufanya vizuri katika fani zao kwa kuwakumbusha kuzingatia maadili ya kazi zao
Sambamba na Hayo ametoa
wito kwa wadau mbali mbali kuunga mkono juhudi za Serikali kusaidia upatikanaji
wa kundi bora la wanawake lenye kujitegemea katika kuboresha na kuinua uchumi
katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Nae Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Zanzibar Mhe Juma Makungu Juma amesema Serikali inatambua mchango wa
wanawake wahasibu nchini katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na
uaminifu mkubwa hivyo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na TAWCA ili kufika malengo
ya kuanzishwa kwa Chama hicho.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Baraza la Uongozi la TAWCA, CPA Neema Kiure amesema lengo la kongamano hilo
ni kuwajengea uwezo na kupeana taaluma na ujuzi kwa wahasibu wanawake ili
kuchochea mabadiliko ya kiutendaji na kimaendeleo katika kada ya uhasibu
nchini.
Amesema TAWCA imekuwa
ikitoa elimu kwa wajasiriamali wanawake juu ya kutunza kumbukumbu za biashara
na namna ya matumizi mazuri ya mikopo wanayopatiwa ili waweze kupata matokeo
yenye tija na faida zaidi.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji
wa Bodi ya Taifa wahasibu na Wakaguzi wa hesabu Tanzania(NBAA) CPA Pius Maneno
amesema taaluma ya uhasibu inakuwa kwa kasi Tanzania ambapo hadi kufikia mwaka
2024 wahasibu wanawake waliosajiliwa wamefikia asilimia 34% na ambao wanasaidia
kufikisha elimu ya utunzaji wa fedha kwa wafanyabiashara na wajasiri amali
nchini.
CPA Maneno amesema kazi
kubwa inayofanywa na TAWCA ni kudhibiti na kusimamia taaluma ya uhasibu kwa
kuwapatia ujuzi na nyenzo wahasibu wanawake za kuweza kuwafikia wanawake na
wasichana nchini kuwapa elimu ya biashara na ujasiriamali ili kujikwamua kimaisha.
No comments:
Post a Comment