Na, Mwandishi wetu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu Zanzibar yana lengo ya kuwaongezea uwelewa viongozi wa umma na wananchi kuhusu umuhimu wa maadili, Utawala wa Sheria, haki na usawa, uadilifu na uwajibikaji pamoja na kuzuia rushwa na ubadhirifu wa mali za Umma.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika
Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu Zanzibar yaliyofanyika
katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais amesema Taasisi zinazosimamia Utawala bora ikiwemo Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala bora zimepiga hatua na zinaendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kudhibiti mianya ya rushwa, upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida kwa kila mwezi zinazopelekwa katika kila Wizara, Idara na Taasisi zinatumika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais amesema kuongezeka kwa idadi ya hati safi za ukaguzi ni uthibitisho tosha unaoonesha kuwepo kwa uwajibikaji katika usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma uliopelekea kuimarika kwa huduma bora na ustawi wa jamii ikiwemo Miundombinu, Elimu, huduma za Afya, Umeme na Maji.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewakumbusha viongozi wote kufanya kazi zao kwa kufuata sheria na miongozo ya kazi zao na kutoa maelekezo kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Mamlaka nyengine husika kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu zinazostahiki kwa mujibu wa sheria viongozi wote wanaolalamikiwa kuvunja maadili katika nchi.
Nae waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Mwalimu Haroun Ali Suleiman
amesema ni jukumu la Viongozi na watumishi wa Umma kuwa na Uzalendo,
Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu ambavyo ndio vigezo na mihimili ya Utawala bora wenye kufuata
sheria na maadili.
Akiwasilisha maada katika
maadhimisho hayo juu ya umuhimu wa
usimamizi wa Rasilimali za umma na Mapambano dhidi ya Rushwa katika kuimarisha
Utawala Bora Mhe. Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim ameelezea makosa mbali mbali ya
kisheria ambayo viongozi na watumishi wa umma wanatakiwa kujiepusha nayo
ikiwemo kutoa na kupokea rushwa, usimamizi na matumizi mabaya ya rasilimali za Umma pamoja na matumizi mabaya ya madaraka .
Jaji Ibrahim amesema Viongozi na watumishi wa Umma ni vyema kujiepusha na yale yote yaliyotajwa katika kifungu cha 18, Sheria namba 4 ya mwaka 2015, Sheria ya maadili ya Viongozi wa umma Zanzibar ili kuendelea kuwa na viongozi bora wenye kufuata sheria, miongozo na Maadili ya Viongoziwa Umma kwa maslahi mapana ya nchi.
Maadhimisho ya siku ya Maadili na
Haki za Binaadamu hufanyika kila ifikapo Disemba 10 ya kila mwaka ambayo
yanaenda sambamba na siku ya mapambano dhidi ya rushwa ambayo hufanyika kila
ifikapo Disemba 9 ya kila mwaka ambapo kwa upande wa Zanzibar maadhimisho hayo
hufanywa sambamba Disemba 10 ambapo hubeba maudhui yenye mnasaba na siku hizo.s
No comments:
Post a Comment