Mhe, Hemed Ashiriki siku ya Maadhimisho Siku ya Maadili

 

Na, Mwandishi wetu



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu Zanzibar  yana lengo ya kuwaongezea uwelewa viongozi wa umma na wananchi kuhusu umuhimu wa maadili, Utawala wa Sheria, haki na usawa, uadilifu na uwajibikaji pamoja na kuzuia rushwa na ubadhirifu wa mali za Umma.

Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu Zanzibar yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba.

 Amesema kila Taasisi na mwanachama kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha anatekeleza misingi ya utawala bora ili kuimarisha uadilifu, haki za Binaadamu na kuzuia rushwa ili Serikali iweze kufikia malengo yake ya kuwapatia maendeleo wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Taasisi zinazosimamia Utawala bora ikiwemo Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala bora zimepiga hatua na zinaendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kudhibiti mianya ya rushwa, upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha za matumizi ya kawaida kwa kila mwezi zinazopelekwa katika kila Wizara, Idara na Taasisi zinatumika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais amesema kuongezeka kwa idadi ya hati safi za ukaguzi ni uthibitisho tosha  unaoonesha kuwepo kwa uwajibikaji katika usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma uliopelekea kuimarika kwa huduma bora na ustawi wa jamii ikiwemo Miundombinu, Elimu, huduma za Afya, Umeme na Maji.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewakumbusha viongozi wote kufanya kazi zao kwa kufuata sheria na miongozo ya kazi zao na kutoa maelekezo kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Mamlaka nyengine husika kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu zinazostahiki kwa  mujibu wa sheria viongozi wote wanaolalamikiwa kuvunja maadili katika nchi.

Nae waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Mwalimu Haroun Ali Suleiman amesema ni jukumu la Viongozi na watumishi wa Umma kuwa na Uzalendo, Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu ambavyo ndio vigezo  na mihimili ya Utawala bora wenye kufuata sheria na maadili.

 

 

 Mhe. Harun amesema katika kuhakikisha elimu ya Maadili na Utawala bora inawafiki viongozi, watumishi wa umma na wananchi wote, Wizara yake imeanzisha Online TV ambayo inalenga kufikisha Taaluma kwa kuandaa Vipindi vitakavyoonesha utendaji kazi wa Wizara na Taasisi  zote za Serikali na Binafsi ili kutanua wigo na uwelewa mpana wa Haki za Binaadamu nchini.

 

Akiwasilisha maada katika maadhimisho hayo  juu ya umuhimu wa usimamizi wa Rasilimali za umma na Mapambano dhidi ya Rushwa katika kuimarisha Utawala Bora Mhe. Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim ameelezea makosa mbali mbali ya kisheria ambayo viongozi na watumishi wa umma wanatakiwa kujiepusha nayo ikiwemo kutoa na kupokea rushwa, usimamizi na matumizi mabaya ya rasilimali za Umma  pamoja na matumizi mabaya ya madaraka  .

Jaji Ibrahim amesema Viongozi na watumishi wa Umma ni vyema kujiepusha na yale yote yaliyotajwa katika kifungu cha 18, Sheria namba 4 ya mwaka 2015, Sheria ya maadili ya Viongozi wa umma Zanzibar ili kuendelea kuwa na viongozi bora wenye kufuata sheria, miongozo na Maadili ya Viongoziwa Umma kwa maslahi mapana ya nchi.

Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binaadamu hufanyika kila ifikapo Disemba 10 ya kila mwaka ambayo yanaenda sambamba na siku ya mapambano dhidi ya rushwa ambayo hufanyika kila ifikapo Disemba 9 ya kila mwaka ambapo kwa upande wa Zanzibar maadhimisho hayo hufanywa sambamba Disemba 10 ambapo hubeba maudhui yenye mnasaba na siku hizo.s

 

 

 

 


Wajasiriamali wa TASAF waeleza Mafanikio ya Mpango huo Zanzibar

Na, Mwandisho.   Unguja. Wajasiriamali waliopo kwenye vikundi vya Mpango wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wameeleza namna mpango huo ulivyowa...