Ujio wa Mufti ISMAIL BIN MUSSA MENKI ZANZIBAR KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

 


Na.Fatma Rajab



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Ujio wa Mufti ISMAIL BIN MUSSA MENKI kutoka nchini  Zimbabwe umetoa fursa kwa Zanzibar kujitangaza zaidi kiutalii kupitia Utalii wa Maadili yani (HALAL TOURISM) uliojikita zaidi katika sheria na misingi ya Uislamu.

Ameyasema hayo katika hafla ya JUKWAA la UWEKEZAJI wa Utalii halali (HALAL TOURISM) lililofanyika katika Viwanja vya  Hotel ya Verde Mtoni jijini Zanzibar.

Amesema uwepo wa Mufti Menki nchini umeitangaza Zanzibar kiutalii na kupata fursa ya kujifunza mambo mbali mbali kupitia Jukwaa la Utalii wa maadili lililotoa fursa kwa Mufti huyo na ujumbe wake aliokuja nao katika kuukumbusha umma umuhimu wa mikusanyiko ya dini na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya Allah.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu mbali mbali ikiwemo ya barabara, Viwanja vya ndege na Bandari ambavyo vinachochea ukuwaji wa sekta ya Utalii nchini sambamba na kuviboresha vivutio vya utalii ili kuendelea kujitangaza kiutalii hasa katika maeneo ya kihistoria, kutangaza mila, silka na tamaduni njema zinazofuata mwenendo mzima wa kiislam ikiwemo Ibada, mavazi, ukarimu na ushirikiano katika jamii.

Aidha, Mhe.Hemed amefahamisha kuwa Serikali kupitia Kamisheni ya Utalii inaendelea kufanya mapitio ya mwisho ya Sera ya Utalii ya Zanzibar ya Mwaka 2017 kwa lengo la kuifanyia maboresho ikiwemo eneo la Utalii wa maadili kwa kuweka mikakati mbili mbali itakayosaidia kukuza utalii wa kiislam hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuahidi Mufti Menki na ujumbe wake kuwa Serikali na waislamu kwa ujumla watayafanyia kazi yale yote waliyojifunza kutoka kwako na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Zanzibar kiutalii hasa katika Utalii wa maadili na kuwahamasisha wataalamu  mbali mbali wa Kiislamu kuja Zanzibar kufanya Tafiti za historia ya kiislam zitakazosaidia kuitangaza dini na  Zanzibar kwa ujumla.

Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe.Mudrik Ramadhan Soraga ameishukuru Kampuni ya Light upon Light kwa kuamua kufanya Jukwaa la Utalii wa maadili Visiwani Zanzibar ambalo litasaidia katika kuitangaza Zanzibar kiutalii na kutanua wigo kwa wageni wengi zaidi kuitembelea Zanzibar.

Mhe. Soraga amesema Jukwaa la Utalii wa maadili ni muhimu katika maendelea ya Zanzibar na kila kilichojadiliwa katika Jukwaa hilo kinalenga katika kuiendeleza Zanzibar kiutalii na kuifanya kuwa Kituo kikubwa cha Utalii Barani Afrika, hivyo atahakikisha kuwa Wizara inachukua juhudi za maksudi kuviboresha vivutio vya utalii na kuanzisha vipya ili kuweza kufikia malengo waliojiwekea.



Kwa upande wake Mufti ISMAIL BIN MUSSA MENKI kutoka nchini Zimbabwe ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wazanzibari kwa ujumla kwa mapokezi ya heshima, upendo na ukarimu walionaompatia yeye na ujumbe wake jambo linalompa faraja ya kuendelea kuitembelea tena Zanzibar na kuahidi kutangaza mazuri yote waliyojifunza Zanzibar .

Amesema kila binaadamu ana wajibu wa kuzitumia neema alizojaaliwa na Allah katika kuisimamia Dini ya kiislam na kuwa tayari kutoa neema hizo kwa ajili ya kuwasaidia wasio na uwezo na wenye mazingira magumu kwa kutambua hilo ndio lengo la kuletwa kwake Duniani kuja kumtumikia Allah (S.W).

Mufti Menki amesema miongoni mwa Ibada anazotakiwa kufanya muislamu ni kufanya kazi ya halali kwa kufuata misingi ya Dini ya kiislamu jambo litakalosaidia waislamu kuishi kwa upendo na kusaidiana pamoja na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

 


No comments:

Post a Comment

Wajasiriamali wa TASAF waeleza Mafanikio ya Mpango huo Zanzibar

Na, Mwandisho.   Unguja. Wajasiriamali waliopo kwenye vikundi vya Mpango wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wameeleza namna mpango huo ulivyowa...