Na. Asia Makame
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeanzisha mpango wa kunusuru Kaya Masikini (PSSN II)
ili kupunguza umasikini uliokisiri katika Kaya mbali mbali Tanzania Bara na
Zanzibar.
Ameyasema hayo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Tathmini ya mwisho ya kupima matokeo ya mpango wa kunusuru
kaya masikini kipindi cha pili ( PSSN II )Tanzania katika Ukumbi wa Sheikh
Idris Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Amesema Mpango huo
unaotekelezwa ndani ya Awamu ya Tatu ya TASAF
unalenga kuziwezesha kaya zinazoishi katika umasikini uliokithiri
kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu na kuondokana na
umasikini kwa kuimarisha uchumi wao kwa faida ya vizazi vijavyo na Taifa kwa
ujumla.
Mhe. Hemed amesema kaya za
walengwa hupatiwa ruzuku ya msingi pamoja na mafunzo ya stadi za ujasiriamali
na mbinu za kuunda vikundi endelevu vya kuwekeza katika shuguli mbali mbali za
kiuchumi ikiwemo kilimo na biashara
Aidha Makamu wa Pili wa
Rais amesema kuwa kaya za walengwa
hunufaika na fursa za ajira za muda mfupi na kujipatia kipato kwa kushiriki
katika miradi mbali mbali ya maendeleo katika jamii kwa lengo la
kuhakikisha wanawasimamia vyema watoto
wao katika kupata elimu na afya bora ili kujenga ustawi mzuri wa familia zao
Sambamba na hayo Mhe.Hemed
amesema kuanzia mwaka 2000 hadi mwezi Agast 2024 Serikali imeweza kuzisaidia
kaya za walengwa wapatao 1,450,000 ambao wameweza kujikwamua kutoka katika hali
ya umasikini uliokithiri na kuweza kujitegemea kimaisha
Mhe. Hemed amezitaka Afisi
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na Afisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania
kuhakikisha Tathmini inayofanywa inatoa Takwimu zenye ubora zitakazoonesha taswira halisi ya hali ilivyo
na kuisaidia Serikali kuona maeneo
ambayo yamefanya vizuri zaidi na maeneo ambayo yanahitaji kuongezewa mkazo ili
malengo ya TASAF yaweze kutimia
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratib na Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu Mhe. ALI SULEIMAN MREMBO amesema Serikali zimeweka mazingira mazuri ya kuhakikisha Mradi wa kunusuru kaya masikini unafanyika kwa ustadi na uweledi wa hali ya juu na kutoa matokea chanya yatakayowanufaisha Watanzania Wengi kwa kuwakwamua katika mazingira ya umasikini uliokithiri kwa baadhi ya kaya.
Mhe. Mrembo amewataka Wakuu
wa Mikoa na Wilaya Masheha na wananchi kutoa ushirikiano wakati wa kufanyika
kwa zoezi la Tathmini ili kuweza kupata Takwimu sahihi zitakazo iwezesha Serikali
kujipanga zaidi katika kuendelea na utekelezaji wa mpango wa kuzinusuru kaya masikini Tanzania nzima.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji kutoka TASAF Bwana Shedrack Mziray amesema madhumuni ya Kufanyika kwa
Tathmini hio ni kuangalia ni kwa kiwango gani Serikali imeweza kuwasaidia
wananchi wake kupitia uwekezaji ilioufanya katika Mpango wa Kunusuru kaya masikini
Tanzania.
Amesema kupitia mpango huo
miradi Elfu 27 imetekelezwa ikiwemo ajira za muda, kuanzisha vikundi vya kukopa
na kuweka hakiba na kupatiwa mafunzo kwa wajasiri amali ambayo imewanufaisha
zaidi ya walengwa wapatao 662, 374 kwa
pande zote za Muungano.
Mapema Mtakwimu mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Zanzibar Ndugu Salum Kassim Ali amesema kuwa
utafiti huu unatarajiwa kufanyika katika Mikoa kumi na saba (17 ) kwa Tanzania
nzima ili kufanikisha lengo la Serikali la kuwatatulia changamoto wananchi wa
kaya masikini zilizopo nchini Sambamba na kuhakikisha tathmini hii itafanyika
kwa kiwango kilichobora na kinachokubalika kitaifa na kimataifa.
No comments:
Post a Comment