Na.Nafda Hindi, TAMWA ZNZ.
Wanawake wameombwa kuvitumia vyombo vya habari ipasavyo
kwa lengo la kutangaza kazi wanazozifanya katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
Akifungua mafunzo ya siku
moja ya kuwajengea uwezo wanawake viongozi
kupitia mradi wa Zanz Adapt Mkurugenzi wa chama cha Waandishi wa habari
Wanawake Tanzania Zanzibar, TAMWA ZNZ Dkt Mzuri Issa Ali amesema wanawake
wanafanya mambo mengi katika jamii ila bado mchango wao haujatambulika kama
ilivyo kwa wanaume, hivyo kuvitumia vyombo vya habari kutawezesha kutambulika
na kujitangaza kwa haraka hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Amesema historia ya Tanzania
na Zanzibar kwa ujumla haioneshi mchango ama juhudi za wanawake kwa sababu
wanawake bado hawajawa na ujasiri na uthubutu wa kutumia vyombo vya habari kwa
usahihi.
“Wanawake wanafanya mambo
mengi katika jamii na kujitoa zaidi, sasa wakati umefika kueleza changamoto na
mambo yanayowahusu kupitia vyombo vya habari ili kupatiwa ufumbuzi,” Dkt Mzuri.
Mkufunzi katika mafunzo hayo
Saphia Ngalapi amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kutatua
changamoto za kijamii, kwa kuzifikia mamlaka husika kuzitafutia ufumbuzi
baada jamii kuelezea changamoto zao.
‘’Kupitia vyombo vya habari
nyinyi nimashahidi tuanaona hatua zinazochukuliwa kwa wahusika endapo kutatokezea tatizo,” Ngalapi.
Akizungumzia mada inayohusu jinsia amesema wazazi/walezi kuwalea watoto wao katika muktadha wa kijinsia kuhakikisha kila mtoto anapata fursa na haki sawa kama zilivyoeleza katiba zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bila kujali jinsia zao.
Nae Afisa Mawasiliano kutoa
Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP) Munira Iddi Kaoneka amesema wanawake hawana budi
kujiamini na kutumia vyombo vya habari kutangaza kazi wanazofanya ikiwemo
mitandao ya kijamii kwani ujumbe wao hufikia watu wengi na kwa wakati mmoja.
“Mukilima na kuvuna mazao
yenu halafu mukanyamaza kimya nani atajuwa kama muna bidhaa, ila chukuwa video
ukivuna mazao kisha rusha Tiktok weka nambari za simu, soko litakuja na watu
watakutafuta,” Munira.
Wanawake viongozi waliopata
mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuwainuwa kiuchumi kwa kulima kilimo msitu chini
ya mradi wa ZanzAdapt wamesema watayatumia vyema mafunzo hayo kwa kuwa mabalozi
bora wa kuwafunza wengine il kukabiliana na mbadiliko ya tabianchi.
Mradi wa Wanawake na Uongozi
katika kukabiliana na mabadilio ya tabianchi (ZanzAdapt) unatekelezwa kwa pamoja na Chama
cha Waandishi Wahabari Wanawake Tanzania TAMWA ZNZ, Jumuiya ya Misitu Pemba
(CFP) na Jumuiya ya Misitu Kimataifa (CFI) kwa kushirikiana na ubalozi wa
Canada.