Na. Mwandishi Wetu.
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Nd. Soud Said Ali
amesema Shirika la Biashara Zanzibar limeridhishwa na kazi ya uimarishaji wa
zao la karafuu inayofanywa na Chuo cha Mafunzo Zanzibar.
Mkurugenzi Soud amesema hayo katika hafla ya kukabidhi
vifaa kwa ajili ya uatikaji miche ya mikarafuu Chuo cha Mafunzo Langoni.
“Shirika
linaridhishwa na kazi nzuri mnayofanya Chuo cha Mafunzo ya kuimarisha zao la karafuu
na Shirika litaendelea kuunga mkono ili kuhakikisha zao hili linarudi katika
asili yake”. Alifahamisha Mkurugenzi Soud,
“Chuo
cha Mafunzo mna maeneo mazuri kwa upandaji wa mikarafuu na nguvu kazi ya
kutosha hivyo kwa pamoja tunaweza kufanikiwa katika jitihada hizi za kuimarisha
zao la karafuu na kuongeza uzalishaji”. Alisisitiza Mkurugenzi Soud.
Aidha juhudi hizo za umiarishaji wa zao la karafuu zitaendelea kwa utoaji wa vifaa vya uatikaji wa miche ya mikarafuu kwa vitalu vya wakulima binafsi na Wizara ya Kilimo
Kwa
upende wake Kamishna Msaidizi Chuo Cha Mafunzo Zoni ya Mashamba ACP Amour Naimu
Khamis. amesema kuwa Chuo cha Mafunzo kinashukuru na kuthamini mashirikiano
baina yake na Shirika la ZSTC katika uimarishaji wa zao la karafuu.
Alisema
kuwa, Chuo cha Mafunzo kitatumia vifaa na elimu wanayoipata Kutoka ZSTC katika
kupanda na kuihudumia mikarafuu kwa maslahi ya Chuo, ZSTC na Serikali.
ZSTC
na Chuo cha Mafunzo Zanzibar wameingia katika
makubaliano na mashirikiano ya kuimarisha zao la karafuu kwa kupanda
mikarafuu katika mashamba ya chuo cha Mafunzo, uanzishwaji wa kitalu cha miche
ya mikarafuu, uchimbaji wa visima na
miundombinu ya umwagiliaji.
Katika
hafla hiyo Mkurugenzi Soud alikabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili ya uoteshaji
miche ya mikarafuu ambayo itapandwa katika mashamba ya Chuo cha Mafunzo Langoni
na Kinumoshi.